Utafiti uliyofanywa na shirika la kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ umebaini kuwa zaidi ya asilimia 30 ya vijana katika eneo la Kisauni wameathiriwa na utumizi wa dawa za kulevya na kuchangia ukosefu wa usalama.
Afisa mratibu wa mipango katika Shirika hilo la Kijamii, Hassan Kibwana amesema kuwa idadi hiyo ya vijana ni kati ya umri wa miaka 12 hadi 20 waliyojitosa katika jinamizi la mihadarati na kuchangia usalama duni katika eneo hilo hali ambayo imezorotesha shughuli za kibiashara katika kaunti nzima ya Mombasa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika kongamano la vijana, Kibwana amesema kuwa kuna haja ya jamii kuungana na idara ya usalama, wadau mbalimbali wa kukabiliana na mihadarati pamoja serikali ili kuwanasua vijana hao na kuimarisha usalama kwa kuzingatia maadili mema.
"Tumebaini kuwa idadi ya vijana katika eneo la Kisauni kaunti ya Mombasa wameathirika na mihadarati hasa kati yao ni vijana wa umri wa miaka 12 hadi 20 idadi ambayo lazima itatuliwe kama haraka," alisema Kibwana.
Mwanaharakati huyo wamesema kuwa hatua ya vijana kujiunga na utumizi wa mihadarati imechangia na ukosefu wa maadilifu mema kutoka kwa jamii na swala hilo linafaa kuchukuliwa kwa usawa ili kuwanasua vijana na kuimarisha usalama.