Askofu wa kanisa la Katoliki dayosisi ya Eldoret Cornelius korir ameelezea hofu kuwa watoto wengi wako katika hatari ya kudhulumiwa wakati huu wa likizo.
Korir alisema hali hii inatokana na kupanda kwa gharama ya maisha ambapo wazazi wengi wanatumia muda wao mwingi kutafuta riziki huku wakiwaacha watoto nyumbani.
Akihutubu katika kaunti ya Uasin Gishu, Korir aliwataka wazazi kuajibikia majukumu yao ya ulezi wakati huu wa likizo licha ya hali ngumu ya maisha.
Kulingana na askofu huyu, watoto wengi huwa salama wakati wanapokuwa shuleni kwani walimu huwalinda na kuwatunza ipasavyo kinyume na nyumbani ambapo wazazi wengi hawana muda na watoto wao.
"Tabia hiyo ya wazazi kukosa muda wa kukaa na watoto wao huhatarisha maisha ya watoto ambapo watu wenye tabia ya kudhulumu watoto hutumia nafasi hiyo," alisema Korir.
Kutokana na hali hiyo Korir ametaka wadau wote kushirikiana ili kuwapa watoto mazingira bora wakati huu wa likizo.
Kiongozi huyo alitaka watu ambao hudhulumu watoto kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kulinda watoto.
Korir alidai kuwa ukosefu wa vifaa vya watoto kuchezea wakiwa nyumbani vile vile ni mojawapo wa changamoto ambayo huwafanya watoto kujihusisha na tabia patovu.
“Silaumu watoto ambao walipatikana katika kilabu kimoja mjini Eldoret; nalaumu wadau wote kwa kukosa kushirikiana kuwekea watoto mazingira bora ya kuchezea na maeneo ya watoto kustarehe,”alisema.