Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amewahimiza wakenya kutoka matabaka mbalimbali na hata watalii kutoka mataifa ya kigeni kuzuru Mombasa msimu huu wa Krismasi pasi na kuhofia usalama wao.

Akihutubu katika ufuo wa bahari za Pirates Mombasa Jumatatu alipokuwa akikagua sehemu watakazo kita kambi maafisa wa usalama, Marwa aliwaonya maadui wote wa usalama kuwa yeyote atakayevuruga amani wakati huu ambapo wakenya wanajiandaa kuadhimisha siku kuu ya Krismasi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Marwa pia alisema kuwa serikali imeweka mipango dhabiti ili kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa katika sehemu mbali mbali Pwani ili kupunguza visa vya utovu wa usalama ambavyo mara nyingi ushuhudiwa Mombasa wakati wa likizo.

"Kama serikali tunajua kuwa kuna wale wanopanga kutumia fursa hii kuhangaisha wananchi na kuvuruga amani, lakini natoa onyo la mapema ili mtu akijipata hatiani ajilaumu mwenyewe," alisema Marwa.

Idadi ndogo ya watalii ilishuhudiwa Mombasa mwaka wa 2014 kutoka na mashumbulizi ya kigaidi yaliadhiri sehemu nyingi nchini, lakini idadi hiyo tayari imeongezeka maradufu mwaka huu kufuatia kuimarishwa kwa usalama.