Share news tips with us here at Hivisasa

Ni jambo la kusikitisha unapoona jinsi vijana katika kaunti ya Garissa wanavyojitumbukiza katika janga hili la mihadarati.

Matumizi ya miraa imekuwa ikiongezeka miongoni mwa vijana wa jamii ya wasomali, Garissa na kaskazini mashariki kwa ujumla, huku zaidi ya walio na umri wa miaka 20 na kuelekea chini wakiathirika sana.

Wapo vijana ambao wanajiingiza katika matumizi ya miraa bila kufahamu athari zake.

Zipo athari nyingi kutokana na matumizi ya miraa ambayo vijana wengi wamejitumbikiza kumewapelekea kuchanganyikiwa na kupumbaa kwa ufahamu, hivyo kuhitaji elimu.

Miongoni mwa madhara ya miraa ni kupotoka maadili. Ni kawaida kwa wengi ili wafikie malengo ya kupata watakacho, wana hulka ya kudanganya wengine kwa kuwakopa pesa za kununua nazo miraa. Ili waweze kukubaliwa kupata mikopo hizo, aghlabu wanapokopa hawasemi ukweli kwa kuwa wanataka pesa za kununua miraa, maana wasipotumia ujanja huo, hakuna atakayewakopesha pesa.

Walaji miraa huwa na tabia na mienendo yasiyoridhisha wanajamii kwa kuwa tabia zao ni ya kuogofya na kutamausha.

Wanaotumia miraa husababisha ugomvi na ukosefu wa utangamano na familia yao ikzingatiwa kuwa baadhi yao huja nyumbani wakiwa wamechelewa na kulazimu migogoro ya kifamilia kuzuka kila siku.

Utumizi wa miraa husababisha madhara mbalimbali ya kiafya kama vile magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers) na ukosefu wa haja kubwa (constipation).

Utumiaji wa miraa kwa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini na pia husababisha ubadilikaji wa rangi ya meno au hata vijana kupoteza meno wakiwa na umri mdogo sana, kudhoofika, ufizi kuuma na kutoa harufu mbaya ya mdomo.

Jamii ya wasomali, hususan vijana, wanashauriwa kuacha matumizi ya dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikiathiri nguvu kazi ya taifa na kuwafanya vijana wengi kuishi katika hali hatari na kuendelea kuilalamikia serikali kutowajali na kuwatengenezea miundombinu ya kupiga hatua kimaisha.