Mwakilishi wa wadi ya Gesima Ken Atuti ameipongeza serikali ya kaunti ya Nyamira kwa kujitolea kuimarisha huduma za afya katika kaunti hiyo.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Nyamira, Atuti, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya afya kwenye bunge la Kaunti ya Nyamira, alisema kuwa kamati hiyo ya afya imefanikiwa kuona mapendekezo yake mengi yakitekelezwa na serikali ya kaunti.
Atuti alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo haijashuhudia migomo ya wahudumu wa afya kama kaunti zingine.
"Kama mwenyekiti wa kamati ya afya kwenye bunge la Kaunti ya Nyamira kwa kweli naeza sema kuwa serikali ya kaunti hii imefanya juhudi kuimarisha huduma za afya. Tumeona mapendekezo mengi ya kamati ya afya hasa yakuajiri wahudumu wa afya yakitekelezwa na hata zahanati kujengwa," alisema Atuti.
Aidha, alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka juhudi kuhakikisha kuwa huduma za kliniki tamba za kuwapima wagonjwa zinawafikia wenyeji.
"Sijawahi sikia wahudumu wa afya katika zahanati na hospitali zetu wakishiriki migomo kama wenzao kutoka kaunti zingine. Hata mapendekezo yakujengwa kwa zahanati ili kuwarahisishia wenyeji huduma yameafikiwa,” alisema Atuti.