Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amemlaumu kinara wa Cord Raila Odinga na gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho kwa kumtenga katika uzinduzi wa barabara ya Fidel Odinga licha ya barabara hiyo kuwa katika eneo bunge lake.
Akizungumza eneo la Chaani huko Changamwe siku ya Jumapili, Awiti aliitaja hatua hii kama kumtenga kisiasa baada ya kutangaza azimio lake la kuwania kiti cha ugavana wa kaunti ya Mombasa mwaka 2017.
Awiti alisema kuwa viongozi hao walimtenga baada ya yeye kuwa na ukaribu na rais Uhuru Kenyatta wakati alipokuwa amezuru kaunti ya Mombasa wiki chache zilizopita.
Kauli yake inajiri baada ya Odinga kuzuru Mombasa na kuzindua barabara ya Fidel Odinga katika eneo la Kongowea wiki iliyopita bila yeye kujulishwa.