Uhasama wa kisiasa baina ya Mbunge wa Nyali Hezron Awiti na Gavana wa Mombasa Hassan Joho unaonekana kuzidi kupanuka zaidi huku mbunge huyo akiendelea kushtumu uongozi wa gavana huyo hadharani.
Mbunge huyo wa Nyali alimkosoa Gavana Joho kwa madai kuwa anawanyanyasa wananchi wa kaunti hiyo bila kujali.
Awiti alidai kuwa Joho aliwaagiza wakaazi wanaoishi katika nyumba za makaazi eneo la Khadija kuwa wataondolewa ifikiapo mwezi Aprili ili kupisha ujenzi wa nyumba mpya za ghorofa.
Awiti alikuwa akiongea siku ya Jumamosi katika shule ya msingi ya Khadija alipokutana na wakaazi hao baada ya kualikwa ili kujadili swala hilo.
Akiwahutubia wakaazi hao, Awiti alisema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa mpango huo unafutiliwa mbali na kuwaagiza kutoondoka katika eneo hilo.
“Nyinyi mna haki ya kuishi hapa na kama kuna mabadiliko yoyote yanafanyika, lazima kwanza mshauriwe. Hatua ambayo gavana anataka kuchukua sio sawa na siwezi nikakubali hayo,” alisema Awiti.
Awiti alisema kuwa Joho hakumfahamisha kama mbunge wa eneo hilo kwamba kuna mradi wa ujenzi unaopaniwa kuanzishwa katika eneo hilo na kutaja hatua hiyo kama dharau.
Wakati huo huo, aliongeza kuwa alimuandikia barua gavana lakini hakuna majibu aliyopewa hadi kufikia sasa.
“Mimi kama mbunge nilimuandikia barua lakini sijapata majibu kuwa kuna mradi wa maendeleo unaofanyika hapa,” aliongeza Awiti.
Eneo la makazi la Khadija Estate lina takriban nyumba 100, ambapo watu wanaoishi humo hulipa kodi kila mwisho wa mwezi.
Wakaazi wa eneo hilo wameitaka serikali ya kaunti kusitisha mpango huo wa kubomoa nyumba hizo.