Waziri wa Utalii Najib Balala ametaka serikali za Kaunti za Mombasa, Kilifi, Kwale na Lamu kubuni sheria kuthibiti watu wanaozuru bahari kama waelekezi wa watalii. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Babala alisema kuwa sheria ya sasa inampa kila mtu ruhusa kutalii baharini wakati wowote jambo ambalo huenda likasababisha hasara kwa sekta hiyo kwani wageni wengi wamelalamika kuibiwa baharini na watu wanaojifanya mabaharia.

''Lazima sheria iwekwe ili wageni wasiwe na hofu bali wajihisi nyumbani, hatuwezi kubali mambo ya wizi kwa wageni kuendelea,'' alisema Balala. 

Balala aidha alisema kuwa tayari amezungumza na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho na kuafikiana kuhusu mikakati ya kuuboresha utalii mjini humo ikiwemo kuhakikisha kuwa usafi wa mji unaimarishwa ili kuwavutia wageni wengi.

''Tumekubaliana na Gavana Joho, tunataka bahari iwe mahali pa kupumzika na kupunga hewa safi kwa wageni wetu,'' alisema Balala.

Waziri huyo pia alidokeza kuwa wizara yake itafanya kazi kwa karibu na wadau wa sekta ya utalii pamoja na mashirika mbali mbali ikiwemo Jumuiya ya Kaunti za Pwani kama njia moja ya kuleta suluhu kwa changamoto zinazokumba sekta hiyo.

Bahari ya Pwani hushuhudia zaidi ya wahudumu 10,000 kila siku miongoni mwao wapiga picha, wenye mashua, wauza matunda, wafanyibiashara wa nguo na walekeze wa wageni.