Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Waziri wa utalii Najib Balala amewataka wenye hoteli nchini kupunguza ada wazanaotoza wageni wanaotembelea hoteli zao ili kuwawezesha hata wenye mapato ya chini kuzuru hoteli hizo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, waziri huyo alitaja ughali wa ada unaotozwa wageni katika baadhi ya hoteli nchini kama kikwazo ambacho kinawazuia Wakenya wengi kutalii nchi yao.

"Nanyi wenye hoteli msiwanyanyase wananchi kwa kuweka bei ghali, si kila mtu ana uwezo wa kutoa pesa kama wanavyotoa wageni kutoka nje. Wekeni bei itakayomruhusu mkenya kutalii nchi yake," alisema Balala.

Balala vilevile alisema kuwa serikali itaboresha ujenzi wa kivukio cha Likoni ili kurahisisha safari katika kivukio hicho na kuimarisha shughuli za utalii nchini.

Kauli ya waziri huyo inajiri siku chache tu baada ya Wakenya kulalamika katika mtandao wa kijamii kwa kile walikitaja kama kudunishwa hadhi katika baadhi ya maeneo ya utalii nchini.

Wengi wao walidai kuwa wanapewa huduma mbovu ikilanganishwa na watalii wa kigeni.