Waziri wa utalii Najib Balala amewataka kila wahusika na washika dau kwenye masuala ya kitalii nchini kuchukua nafasi yao kuhakikisha kuwa utalii unaboreshwa katika eneo la pwani na.
Aidha ametaka shida inayoendelea kulikumba shirika la feri kupata suluhu ya kudumu ili kuwaepusha wageni na masaibu ya kukwama kwenye milolongo kwenye kivuko cha feri cha Likoni.
Akiongea siku ya Jumatatu kwenye mkahawa mmoja katika eneo la South Coast Ukunda, Balala alisema kuwa utalii umerudi chini katika eneo hilo kwa sababu ya mitafaruku ya mara kwa mara ambayo ipo kwa sasa kwenye kivuko hicho.
Aliongeza kuwa sharti kuwepo ushirikiano kati ya washika dau pamoja na shirika la feri ili kurejesha hadhi ya jiji la Mombasa kwenye kilele cha mapokezi ya watalii, ikizingatiwa kuwa jiji hilo limetoka kutambulika kwa masuala ya kitalii kwenye majukwaa ya kimataifa.
Waziri huyo alisema kuwa atafanya kila awezalo kwa kushirikiana bega kwa bega na wahusika kwenye sekta ya kitalii kuimarisha hali ya utalii kwenye eneo la Pwani kama njia mojawapo ya kuwapa moyo wakazi wa maeneo hayo ambao kwa kina wanategea upataji wa riziki kutokana na shughuli za kitalii.
Mkutano huo uliandaliwa mahusus kwa washika dau wa sekta ya utalii, na ulikuwa mkutano wa kwanza Balala ameandaa rasmi katika eneo la Pwani kuzungumzia masuala ya kitalii tangu kuteuliwa kuchukua nafari ya uwaziri na Rais Uhuru Kenyatta kwenye mabadiliko yaliyofanyika kwenye baraza la mawaziri mapema mwezi huu.