Share news tips with us here at Hivisasa

Baraza la maimam na wahubiri nchini limemwahakikishia mkurugenzi mkuu wa kamati ya kudhibiti filamu nchini Ezekiel Mutua kuwa wapo tayari kuunga mkono vita dhidi ya vipindi na filamu potovu zinazoonyeshwa katika vituo vya televisheni na kuwekwa hewani katika vituo vya redio nchini.

Baraza hilo limesema kuwa vipindi vibaya na filamu katika vituo vya redio na televisheni vimekuwa chanzo cha kuwa na maadili mabaya miongoni mwa watoto wadogo pamoja na vijana ambao tayari wamebaleghe.

Akiongea siku ya Jumatano kwenye mkutano na baraza hilo la CIPK pamoja na mkurugenzi wa KFCB, mwenyekiti wa baraza la CIPK Mohammed Khalifa alisema kuwa wataunga mkono sheria na utaratibu wowote ambao unalenga kurekebisha mienendo mibaya kwenye jamii.

Kwa upande wake, Mutua aliwataka viongozi hao kutoa ujembe kwenye misikiti na madrasa mahusus kuwafikia vijana na watoto wadogo ili jamii kwa jumla iwe na vizazi vya kuheshimu maadili na kulea kizazi chenye mwelekeo mwema.

Mutua pia alisema kuwa sheria hiyo si adui kwa vyombo vya habari bali ni kwenye juhudi za kuhakikisha kuwa nchi inakuza maadili na nidhamu, na kusema kuwa wale wanaoendeleza uvumi kuhusiana na utaratibu na sheria hiyo wanafanya hivyo kupotosha na kwa maslahi ya kibinafsi.

Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kuharamishwa kwa matangazo ya biashara ya kutangaza pombe na sigara, kupeperushwa kwa filamu zenye picha za kimahaba miongoni mwa mengine.