Baraza la Maimam na Wahubiri wa humu nchini limempa Rais Uhuru Kenyatta makataa ya siku tano kuishinikiza idara ya usalama pamoja na wizara ya usalama wa ndani nchini kutoa ripoti kuhusu mauaji ya watu 12 waliopatikana wamezikwa katika kaburi moja.
Kwenye mkao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa amesema kwamba ripoti ya kupatikana kwa miili ya wakenya wasio kuwa na hatia wakiwa imeuwawa ni ya kusikitisha mno.
Sheikh Khalifa, ambaye pia ni kiongozi wa dini ya Kiislam, amesema kwamba rais anafaa kuishinikiza idara ya usalama kuwatia nguvuni waliohusika na mauaji hayo mjini Mandera, na hatua kali dhidi ya wahusika kuchukuliwa ili kusitisha visa vya kupotea kwa watu kila uchao.
Wakati uo huo, viongozi hao wameikashfu serikali kwa kutumia fedha nyingi katika idara ya usalama huku wakenya wasiokuwa na hatia wakiuwawa na watu wasiojulikana.
"Tunamtaka Rais Kenyatta kujitokeza waziwazi na kuishinikiza idara ya usalama inayoongozwa na Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet kutoa ripoti ya mauaji ya watu zaidi ya 12 kule mjini Mandera waliopatikana wamezikwa katika kaburi moja na waliohusika bado hawajajulikana, hilo tunataka kuelezwa mara moja," alisema Sheikh Khalifa.
Kauli ya kiongozi huyo wa dini ya kiislam imejiri siku chache tu baada ya miili ya watu zaidi ya 12 ikipatikana katika kaburi moja huko mjini Mandera, baada ya familia ya watu hao kuwasilisha ripoti kwa idara ya usalama kuhusu kupotea kwa watu wao.