Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku mitihani ya kitaifa ya KCPE ikikamilika siku ya Alhamisi, baraza la mitihani nchini limeshtumiwa kwa kushindwa kudhibiti udanganyifu wa mitihani ya kitaifa.

Kulingana na afisa mkuu wa shirika la maji na ufanisi Hamisa Zaja, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi wameshiriki udanganyifu wa mitihani ya kitaifa kutokana na kuzembea kwa maafisa wa baraza hilo.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Hamisa alisema kwamba lazima baraza hilo lijizatiti zaidi katika usimamizi wa mitihani ili kuona kwamba visa vya udanganyifu wa mitihani vinasitishwa kwani hatua hiyo huenda ikadidimiza sekta ya elimu nchini.

"Baraza la mitihani nchini limeshindwa kuibuka na mbinu za kuzuia visa vya udanganyifu wa mitihani na hali hii imeliabisha taifa hili ulimwenguni, na tunapendekeza baraza hili lichukue hatua za dhrarura kubadilisha mfumo wake kabla watahiniwa wa mitihani hiyo mwaka ujao kuharibikiwa zaidi," alisema Hamisa.

Wakati huo huo amewataka wazazi kuchunguza mienendo ya watoto wao ili kuwaepusha na kuwaonya kutojihusisha na baadhi ya watu flani wanaolenga kuzipotosha ndoto zao katika siku za usoni ili kuona kwamba watahiniwa wanafanya vyema katika mitihani yao.

Hatua hiyo imejiri baada ya kushuhudiwa visa vingi vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE kote nchini kutokana na kusambazwa kwa makaratasi ya mitihani hiyo.

Baraza la mitihani nchini KNEC lashutumiwa kwa kuchangia udanganyifu wa mitihani ya kitaifa nchini.