Share news tips with us here at Hivisasa

Baraza la wazee limeundwa katika Lokesheni ya Jibana, eneo bunge la Kaloleni kaunti ya Kilifi ili kuchunguza tuhuma kuwa eneo hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo ni chimbuko la vuguvugu la Mombasa Republican Council MRC.

Mbunge wa Kololeni Gunga Mwinga amesema kuwa kuundwa kwa Baraza hilo kunalenga kujenga uhusiano mwema baina ya wakazi wa eneo hilo na Serikali tawala.

Gunga amehoji kuwa eneo hilo limepoteza hadhi yake kwa madai kuwa ni miongoni mwa maeneo yaliyo na wafuasi wa MRC jambo linalotilia shaka shughuli za kiserikali.

“Tunataka wazee hawa kukamilisha uchunguzi wao na kutueleza iwapo kweli MRC bado iko Pwani kwani sisi tunajua hakuna kundi kama hilo watu wa Pwani wanadumisha usalama,” alisema Gunga katika mkutano wa amani na wazee hao katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumamosi.

Ni hivi majuzi tu ambako washukiwa 42 wa vuguvugu la MRC walikamatwa katika kaunti ya Kwale, baadhi yao wakiwa washukiwa wanaotoka Lokesheni ya Jibana.