Baraza la wazee kaunti ya Mombasa wameunga mkono juhudi za rais Uhuru Kenyatta za kusaidia kutatua mizozo ya ardhi katika kaunti hiyo.
Wazee hao wanasema tangu rais Kenyatta aingie uongozini mwaka wa 2013, wana furaha kuwa ameonyesha nia ya kumaliza mizozo ya ardhi miongoni mwa wakaazi wa pwani kwa kutoa hati miliki.
Akiongea katika mkutano na wanahabari ofisini mwake mjini Mombasa siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa baraza hilo Mohamed Jahazi alisema kuwa wana matumaini kuwa shughuli ya kupoeana hati miliki kwa maskwota wa shamba la waitiki Likoni itasaidia.
“Tumeita mkutano huu kumshukuru rais wetu kwa juhudi zake, na shughuli inayotarajiwa ya kupeana hati miliki huko Likoni ni ishara wazi kuwa anawajali wapwani,” alisema Jahazi.
Pia vile vile wazee hao walisema kuwa wameona mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali mkoani pwani kutokana na uongozi wa rais Kenyatta ikiwa ni pamoja na afya, barabara na kadhalika.
Baraza la wazee kaunti ya Mombasa lilianzishwa rasmi machi mwaka wa 2014 kwa lengo la kushirikiana na mashirika ya umma pamoja nay ale ya kibinafsi kusaidia kukabiliana na matatizo mbalimbali katika jamii kama vile maswala ya amani na pia utamaduni.