Bei ya mboga katika soko la wakulima mjini Nakuru imeteremka, huku bidhaa hizo zikionekana kuwa nyingi zaidi kwenye soko za eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wauzaji walioongea na mwandishi huyu walisema mvua inayoendelea kunyesha imechangia kukua kwa mboga kwa wingi, hivyo basi kulazimisha bei kuteremka.

Gunia la kilo tisini la mboga lililokuwa likiuzwa kwa shilingi 1,500, sasa lauzwa kwa shilingi 1,000, huku bei hiyo ikitarajiwa kushuka zaidi siku chache zijazo. 

Noar Ayub,  ambaye anawasimamia wauzaji mboga alisema kuteremka kwa bei ni kawaida wakati bidhaa zinapokua nyingi kwenye soko. 

"Kuteremka kwa bei ni kawaida wakati bidhaa zinapo rundikana kwenye soko, tunatumai bei itaimarika karibuni," alisema Ayub.

Mary Wangare, mfanyibiashara wa mboga naye alisema hali hiyo ni ya mda tu kwani mvua ikiendelea zaidi huenda ikaathiri bei kwani mboga pia zitaathiriwa.

"Sahi mboga iko kwa wingi, lakini mvua ikiendelea kunyesha sana itaharibu hizo mboga pia na kusababisha uhaba hivyo basi kupanda kwa bei tena," aliongezea.