Hatimaye wanafunzi kumi na watano wanaotoka kwenye familia maskini na waliofanya vyema kwenye mtihani wa darasa la nane wamepata sababu yakutabasamu baada ya benki ya Equity tawi la Keroka kuwafadhili kupata elimu ya shule za upili kupitia wakfu wa ‘wings to fly’.
Akihutubu wakati wa hafla hiyo kule Keroka siku ya Alhamisi, mbunge wa Nyaribari Masaba Elijah Moindi alizipa changamoto benki zingine kuiga mtindo huo, huku akihoji hazina ya maendeleo bunge CDF itawafadhili wanafunzi wa eneo bunge lake waliopata alama mia nne na zaidi.
“Hatua ya benki ya Equity kuendelea kuwafadhili wanafunzi werevu wanaotoka katika familia maskini ni mfano unaofaa kuigwa na benki zingine za kibiashara, na kwa sababu ya changamoto ambazo Equity imenipa leo, nami nitawafadhali wanafunzi waliopata alama 400 na zaidi kupitia kwa hazina ya CDF,” alisema Moindi.
Kwa upande wake meneja msimamizi wa mauzo wa benki hiyo tawi la Keroka Robert Abere aliwahimiza wanafunzi walionufaika na ufadhili huo kutia bidii masomoni, huku akiongezea benki hiyo itaendelea kuwafadhili wanafunzi zaidi kujiunga na shule zakitaifa.
“Ni himizo langu kwenu wanafunzi kuendelea kutia bidii masomoni kwa maana taifa hili litahitaji huduma zenu siku za mbeleni na sisi kama benki tutaendelea kufadhili wanafunzi wengi zaidi kwa maana kufikia sasa tumefanikiwa kuwateua wanafunzi 77 ili kupata ufadhili,” alihoji Abere.