Wanafunzi watano wanaotoka kwenye familia maskini na waliofanya vyema katika mtihani wa darasa la nane mwaka jana wamepata sababu yakutabasamu baada ya benki ya KCB kujitolea kufadhili masomo yao.
Akihutubu kwenye hafla ya kuwapokeza wanafunzi hao hundi ya shillingi elfu 283,218, meneja wa benki hiyo tawi la Nyamira Peterson Morara alisema kuwa walichukua hatua hiyo ili kuwasaidia wanafunzi werevu wanaotoka katika familia maskini kupata elimu.
"Tumechukua hatua ya kuwapa ufadhili wa kifedha wanafunzi hawa kwa kuwa kama benki, tunataka kuhakikisha wanafunzi werevu wanaotoka katika familia maskini wanapata nafasi ya kupata elimu ili nao wawe miongoni mwa wale watakaoimarisha uchumi wa Kenya siku za usoni," alisema Morara.
Morara aliongeza kwa kusema kuwa benki hiyo inatarajia kutumia zaidi ya shillingi millioni 2 katika ufadhili wa masomo wa miaka nne kwa wanafunzi walionufaika na mpango huo.
"Tuna furaha kuona kuwa ndoto za wanafunzi hawa hazitazimwa kwa sababu ya ukosefu wa karo, na ndio maana tuna mipango ya kutumia zaidi ya shillingi millioni 2 ili kufadhili masomo ya wanafunzi hawa kwa miaka minne ijayo," aliongezea Morara.
Morara alikuwa akihutubu nje ya makazi ya gavana Nyagarama siku ya Jumatatu wakati wa uzinduzi wa hafla hiyo.