Mwakilishi wa wadi ya Bokimonge eneo bunge la Bomachoge kaunti ya Kisii George Bibao ameomba serikali ya kaunti ya Kisii kutumia pesa ambazo zilitengewa mikasa ya mvua ya gharika (El Nino) kutengeneza daraja la eneo la Tongeri.
Kulingana na mwakilishi huyo daraja hilo lilichukuliwa na maji wiki jana na kushangaa kwa nini serikali haijawajibikia jambo hilo huku watu wakiendelea kusumbuka na kuteseka kuvuka kuenda ng’ambo ingine.
Daraja hilo liko katika kijiji cha Riyabe na Tongeri ambapo kuna hofu ya kuvuka kwani hawana mahala pa kuvukia.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo hilo la Tongeri wakati alitembelea daraja hilo ili kujionea jinsi iliko, mwakilishi Bibao alisema hapo mbeleni kabla ya mvua ya El Nino kuanza serikali ya kaunti hiyo ilikuwa tayari imepanga kutengeneza daraja hilo lakini hadi sasa haijawajibika.
“Kuna pesa zilitengwa kukabiliana na mikasa ya Eli nino lakini daraja hili la Tongeri lilichukuliwa na mvua juma lililopita na halijatengezwa. Naomba serikali kutumia pesa hizo ili kutengeneza daraja maana watu wamesumbuka sana,” alisema Bibao.
“Najua wageni wengi huja nyumbani wakati huu wa sherehe za krismasi na hakuna mahala pa kuvukia. Ikiwa serikali ya kitaifa haijatuma pesa za El Nino sisi wabunge wa kaunti tulipitisha pesa za El nino million 50 naomba zitumike kutoa usaidizi huu sasa,” aliongeza Bibao.