Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wadi ya Bokimonge ameomba jamii ya Kisii na ile ya Maasai kujitenga na vurugu za ukabila na kuishi kwa amani.

Hii ni baada ya jamii hizo mbili kuzua ghasia na vurugu mpakani Narok kuanzia siku ya Jumamosi, ghasia ambazo zilipelekea mtu mmoja kujeruhiwa kwa kudungwa kisu huku shamba moja la miwa ambalo liko katika eneo la Kisii kuharibiwa kwa kuchomwa.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika mpaka wa Kisii na Narok alipotembelea eneo hilo, Bibao aliomba jamii hizo mbili kuacha kuvurugana na kuacha ghasia hizo.

Vurugu hizo zilitulizwa na maafisa wa polisi wa kitengo cha GSU mbao walifika eneo hilo na kufyatua risasi angani na kuwatawanya wakazi hao.

“Naomba jamii hizi mbili kuishi kwa Amani, mapambano ya kila siku hayawezi kutusaidia ila ni kuleta uhalifu ambao hauna msingi wowote,” alisema Bibao.

Aidha, Bibao aliomba wale ambao wanaanzisha vurugu hizo kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Hii si mara ya kwanza jamii hizo mbili kuhusika katika ghasia, ila ni jambo ambalo linajirudia kila wakati huku suluhu halisi ikiombwa kutafutwa kupitia makamishena wa kaunti za Kisii na Narok.