Mamlaka ya kusimamia maswala ya mivinyo na dawa za kulevya nchini sasa imetaka kuondolewa kwa bilibodi zote zilizo na matangazo ya mivinyo kwenye barabara za kitaifa nchini.
Akizungumza na wanahabari mapema Jumatano mjini Naivasha, mwenyekiti wa mamlaka hiyo John Mututho alisema kuwa matangazo hayo yalikuwa yakihitilafiana na sheria zilizowekwa za mivinyo.
Mututho aidha amelalamikia hatua ya tangazo la kampuni ya London Distillers linaloendelea kwenye vyombo vya habari na kusema kuwa amemwandikia kiongozi wa mashtaka kuhusiana na swala hilo.
Wakati huo huo, mbunge huyo wa zamani wa Naivasha ametaka kubatilishwa kwa sheria ya (portable spirits standards) ya mwaka 2009, aliyosema kuwa ina dosari chungu nzima.
Kwa mujibu wake, wafanyibiashara wanaotengeneza mivinyo hiyo kali hawakuwa wakizingatia maswala ya afya huku wakiendelea kuongezea bidhaa tofauti ili wateja wasione kama ni sumu.
“Nacada inashirikiana kwa karibu na mamlaka ya usafiri NTSA ili kuweza kuwanasa madereva walevi kwenye barabara zote nchini haswa msimu huu wa krismasi,” Mututho amesema.