Bodi ya utalii nchini imetoa shukrani kwa jeshi la wanamaji linalolinda usalama Baharini Mombasa, pamoja na lile la KDF kwa mchango wao katika kuimarisha sekta hiyo hapa Kenya.
Bodi hiyo ilisema kuwa jeshi hilo limekuwa macho kuhakikisha kuwa usalama unaimarika katika bahari ya humu nchini, ambayo meli za kitalii hutumia kuingia Mombasa.
Akiongea na wanahabari Bandarini Mombasa siku ya Jumanne, mwakilishi wa bodi hiyo Allan Njoroge, alisema kuwa wameona mabadiliko makubwa tangu jeshi la wanamaji lilipotangaza kuimarisha doria zaidi.
“Tunajua kwamba tulikumbwa na tatizo la kiusalama ambalo liliathiri sekta hii pakubwa. Lakini sasa tunataka kurejesha zile siku ambazo taifa hili lilikuwa likipokea takriban meli 40 kwa mwaka, na tuna imani na jeshi letu,” alisema Njoroge.
Afisa huyo alisema kuwa wamefurahishwa na idadi ya meli za kitalii zinazoendelea kuzuru Mombasa, akitoa mfano wa meli ya Silver Clouds iliyowasili bandarini siku ya Jumanne.
“Meli zinapowasili hapa nchini sisi tunapata nguvu zaidi, na inatuonyesha sote kwamba sekta hii inaendelea kurejesha sifa zake katika soko la kimataifa,” alisema Njoroge.
Wakati huo huo, bodi hiyo ilisema kuwa inafanya mpango wa kuona jinsi watakavyohakikisha kwamba watalii wanaozuru eneo hilo wanakaa kwa muda mrefu kabla ya kuondoka.
Mapema siku ya Jumanne, Bandari hiyo ya Mombasa ilipokea meli ya kitalii iliyobeba zaidi ya watalii 190 kutoka kisiwani Zanzibar.