Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini Salim Mvurya alikosoa vikali hatua ya serikali kuu kuwapokonya walinzi Magavana Hassan Ali Joho wa Mombasa, Amason Jeffa Kingi wa Kilifi na mwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa.

Kwenye kikao na wanahabari siku ya Ijumaa, Mvurya aliitaja hatua hiyo ya serikali kuwa ni vitisho kwa viongozi hasa wa Pwani.

Mvurya aliye pia gavana wa kaunti ya Kwale alisema kuwa hatua ya kuwaondolea viongozi hao walinzi bila ya kuwapa taarifa inaonyesha wazi kuwa serikali kuu haijatilia maanani usalama wa magavana.

Gavana huyo wa Kwale alimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi Nchini Joseph Boinnet kuwarudishia viongozi hao walinzi mara moja, kwani hatua hiyo ni kuhujumu ugatuzi.

“Tunamtaka Inspekta Mkuu wa Polisi Nchini Joseph Boinnet kuwarudishia viongozi hao walinzi kwani hatua hiyo huenda ikasababisha madhara makubwa kwa viongozi hao ambao wanatembea bila walinzi,” alisema Mvurya.

Kwa upande wao wawakilishi wa Bunge la Kaunti ya Kwale, wakiongozwa na kiongozi wa walio wengi bungeni humo Nassoro Mguta, walisema kuwa mrengo wa Jubilee ndio uliohusika na visa vya ukiukaji sheria kwenye uchaguzi mdogo wa Malindi lakini hakuna hata mmoja aliyechukuliwa hatua.

“Tunashangazwa na serikali jinsi ilivyochukua hatua ya kuwaponya viongozi wa Pwani walinzi ilhali wafuasi wa chama cha Jubilee ndio waliohusika katika ukiukaji wa sheria hiyo sio sawa kabisa haki lazima itekelezwe kote,” alisema Nassoro.