Katibu wa Idara ya afya kwenye Kaunti ya Nyamira, amesema kuwa kliniki tamba iliyopokezwa serikali ya kaunti na Bi Margret Kenyatta, itakuwa ikiwahudumia wakazi wa kaunti zote ndogo za Nyamira.
Douglas Bosire aidha alisema kuwa kliniki hiyo tamba itakuwa ikiwashughulikia wakazi, hasa wale wa vijijini huku akiongeza kuwa wahudumu wa afya watalazimika kuwashughulikia wagonjwa majira ya usiku.
"Kliniki hii tamba itakuwa ikiwashughulikia wagonjwa kutoka sehemu zote Kaunti ya Nyamira hasa vijijini bila ya ubaguzi. Wahudumu wa afya sharti wawe tayari kuwashughulikia wagonjwa hata usiku bila yakujali wagonjwa hao wanatoka maeneo gani, kwa kuwa idara ya afya iligatuliwa ili kuwahudumia wananchi," alisema Bosire.
Bosire aidha aliwahimiza wakazi wanaoishi karibu na zahanati kuchukua hatua zakutembelea vituo hivyo vya afya wakati wowote wanapo jihisi kuwa wagonjwa badala yakungoja kupokea huduma za kliniki tamba.
"Kuwepo kwa kliniki tamba huku Nyamira hakumaanishi kuwa wakazi wote watafikiwa na huduma za kliniki hiyo. Ni ombi langu kwa wakazi wanaoishi karibu na zahanati za umma kutembelea vituo hivyo, ili kuwawezesha wakazi wanaoishi mbali kupokea huduma za kliniki tamba,” alisema Bosire.