Huenda wafanyikazi wa afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea kwenye hospitali na zahanati mbalimbali katika Kaunti ya Nyamira wakapata sababu yakutabasamu, iwapo ahadi ya afisa mkuu wa afya kwenye kaunti hiyo kuwaajiri wafanyikazi hao litaafikiwa.
Akihutubu katika Hospitali ya Nyansiongo siku ya Jumanne, afisa mkuu wa afya kwenye kaunti hiyo Douglas Bosire, alisema kuwa idara yake tayari imechukua takwimu za wafanyikazi hao ambao wamekuwa wakihudumu kwenye hospitali na zahanati mbalimbali kwa miaka mitatu bila malipo, ili iwawezeshe kuwaajiri rasmi wafanyikazi hao.
"Tayari tumetoa orodha ya majina ya wafanyikazi watakao faidika kutokana na mpango huu na tutahakikisha kwamba wameajiriwa ili kuwasaidia manesi na madaktari kwenye utendakazi wao," alisema Bosire.
Bosire aidha alisema kuwa wafanyikazi watakao faidika kutokana na mpango huo ni wale wa Nyansiongo, Keroka na Nyamira akihoji wao ndio waliokosa kuajiriwa mwezi Novemba mwaka jana.
"Hawa ni watoto wetu na yafaa tuheshimu mchango wao katika kuimarisha utoaji huduma za afya. Kwa kweli wengine wao wamefanya kazi nasi kwa zaidi ya miaka sita, na ndio maana nikaamua kuwasaidia kwa kushauriana na bodi ya uajiri ya kaunti PSB ambayo imekubali kuwasaidia," aliongezea Bosire.