Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Mvita Abdulswammad Shariff Nassir amedokeza kuwa bunge la kitaifa hivi karibuni litajadili mswaada wa kuwaondoa afisini makamishna wa baraza la kitaifa la mitihani nchini KNEC, baada ya kuibuka udanganyifu katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne.

Nassir alitilia shaka utendakazi wa maafisa hao, na kusema kuwa asilimia kubwa ya wabunge hawana imani na maafisa hao,  hivyo basi uwezekano wao wa kusalia afisini kuwa finyu.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika shule ya msingi ya Tudor kwenye hafla ya kuwaombea watahiniwa wa darasa la nane katika eneo bunge lake, mbunge huyo alipendekeza kuwepo kwa mitihani tofauti itakayopewa kila mwanafunzi ili kuepuka visa hivyo vya udanganyifu katika siku za usoni.

Haya yanajiri baada ya mbunge wa Mbooni Kisoi Munyao kuwasilisha mswaada wa kuvunjiliwa mbali baraza hilo na kuchaguliwa maafisa wapya baada ya baraza hilo kutuhumiwa kushindwa kuzuia visa vya udanganyifu wa mtihani.