Bunge la Kaunti ya Nyamira limelazimika kuahirisha vikao vyake vya mashinani kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.
Akiwasilisha ombi hilo siku ya Ijumaa, Mwakilishi wa wadi ya Nyansiongo, Jackson Mogusu, alisema kuwa kutokana na mvua inayoendelea kunyesha katika eneo hilo, wakazi wengi hawataweza kuhudhuria vikao hivyo.
“Nawaomba wenzangu mkubaliane nami kuhusiana na takwa langu lakutaka kuahirishwa kwa vikao vya bunge mashinani. Kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, itakuwa vigumu kwa wananchi kuhudhuria vikao hivyo,” alisema Mogusu.
Aliongezea, “Wanafunzi tuliokuwa tukiwaalika pia hawataweza kuhudhuria vikao hivyo kwa vile shule zimefungwa.”
Kiongozi wa walio wengi kwenye bunge hilo Laban Masira alipinga pendekezo hilo akisema kuwa vikao vya bunge mashinani havistahili kuairishwa kwasababu zisizo mwafaka.
Alisema kuwa vikao hivyo vinaweza kuahirishwa iwapo kuna hafla muhimu itakayo walazimu wawakilishi wadi kutohudhuria vikao hivyo kama ilivyokuwa wiki jana.
"Hatuwezi kuahirisha vikao vya bunge mashinani eti kwasababu kuna mvua. Kuahirishwa kwa vikao kunaweza tu kutekelezwa kutokana na kutokuwepo kwa wawakilishi wadi,” alisema Masira.
Hata hivyo, idadi kubwa ya wawakilishi waliunga mkono pendekezo hilo lakuahirishwa kwa vikao hivyo hadi mwakani hali iliyomlazimu Spika Joash Nyamoko kuidhinisha pendekezo hilo.