Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Bunge la Kaunti ya Nyamira limepata pigo baada ya kushindwa katika kesi ya kupunguza mishahara ya wafanyikazi wa kaunti.

Akitoa uamuzi wake siku ya Ijumaa, Jaji wa mahakama ya viwanda na masuala ya kikazi kule kisumu Maureen Onyango, aliamuru kutupiliwa mbali kwa barua mpya za uajiri zilizo punguza mishahara ya baadhi ya wafanyikazi katika bunge hilo kwa asilimia 34.

Jaji Onyango aidha aliagiza bunge la kaunti hiyo kuwafidia wafanyikazi walio wasilisha kesi mahakamani, pesa walizotumia kwenye kesi hiyo.

Jaji huyo alisema kuwa hamna sheria inayo ruhusu mwajiri yeyote kubatilisha masharti ya kazi, hasa kwa kupunguza mishahara ya wafanyikazi wake.

Wafanyikazi hao waliowasilisha kesi hiyo kwenye mahakama ya viwanda mwezi Agosti 2015 ni pamoja na afisa wa masuala ya fedha na bajeti Kevin Nyamasege, Karani msaidizi Gilbert Atunga, Afisa mkuu wa masuala ya uajiri Enock Nyakundi, naibu karani wa bunge hilo Simon Onyari, miongoni mwa wengine.