Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Bunge la kaunti ya Nakuru limemrejesha mamlakani kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo George Mwaura baada ya kumwondoa kwenye wadhifa huo kwa njia isiyofaa mwishoni mwa mwaka jana.

Wakiongea katika majengo la bunge hilo Jumatatu, wawakilishi wadi wa TNA na URP walisema baada ya kufanya kikao cha faraghani walikubaliana kumrejesha Mwaura kazini na kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya maendeleo.

Mwaura alibanduliwa kufuatia mkutano uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya kifahari ya Kunste iliyo mjini Nakuru, mnamo Juni 30, 2014, na sasa anasema kwamba amo tayari kufanya kazi na wabunge wote licha ya tofauti za hapa na pale.

Alisema, “Tofauti za kisiasa hazitafanya nishindwe kutekeleza majukumu yangu, kwani hazitasaidia kaunti yetu kiuchumi.”

Aliendelea kusema anaamini “kwamba kaunti ni kubwa kuliko yeyote miongoni mwetu” na atafanya kazi na MCAs wote, iwe walimuunga mkono au la.

Mwaura hata hivyo alisema imefika wakati kwa MCAs hao kukomesha siasa na kufanya kazi kwa manufaa ya wapiga kura waliowachagua.

“Hatufai kuzingatia sana siasa hafifu, ila tunafaa kujituma kuhakikisha kuwa tunahudumia Wanjiku,” aliongeza.

Hata hivyo MCA Waithuki Njane anayewakilisha Naivasha Mashariki na ambaye alichukua usukani baada ya Mwaura kung’atuliwa, amesema atamuunga mkono Mwaura katika maswala yote ya bunge hilo.

Alisema, “Sitakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama. Nimejitolea mwenyewe kuondoka kitini na kufanya kazi kama kikosi kimoja kwa manufaa ya maendeleo.”

Mwaura alirejeshewa wadhifa wake na mahakama ya juu jijini Nairobi wiki jana.