Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la kaunti ya Mombasa limekosolewa vikali kutokana na kupitisha miswada isiyowafaidi wakazi wa kaunti hiyo na kuwanufaisha baadhi ya watu fulani waliyo na ushawishi mkubwa.

Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar Sarai alisema kuwa tangu bunge hilo kubuniwa kupitia ugatuzi bado halijawasaidia wakaazi bali kuwadhulumu na kuwanufaisha watu fulani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Sarai alisema kuwa kamwe viongozi hao wa bunge la kaunti ya Mombasa hawafai kurudishwa uongozini huku akiwashinikiza wakazi kuwabandua mamlakani viongozi hao ili kubalisha uongozi wa kaunti ya Mombasa.

"Viongozi kama hawa hawafai kuchaguliwa tena kwa sababu hao kazi yao kubwa ni kupitisha miswada ya kuwafaidi baadhi ya watu fulani waliyo na ushawishi mkubwa kwenye serikali ya Mombasa, wakati ni sasa kuwaondoa viongozi waliyoshindwa kuwahudumia wakaazi mambo muhimu," alisema Omar.

Wakati uo huo amemkosoa Gavana wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho kwa kuwaongezea kodi wachuuzi wa biashara ndogo ndogo mjini Mombasa sambamba na kuitisha kodi kwa wahudumu wa bodaboda kinyume na sheria za ugatuzi na kusema kuwa hatua hiyo inawakandamiza wakaazi.

"Tunasikitika sana kuona watu wa chini kabisa wanaotegemea biashara zao ndogo ndogo kuwasaidia ndio wanaongezewa kodi na wale wenye shughuli kubwa kubwa hawafanyiwi hivyo, mimi nataka kumwambia Joho kuwa hatua hiyo ni ukandamizaji mkubwa wa wakaazi wa Mombasa," aliongeza Omar.