Hali inatarajiwa kubadilika baada ya pendekezo kutolewa katika bunge la Mombasa kuhusu jinsi ya kudhibiti takataka pamoja na kukinga wananchi dhidi ya kupata maradhi kutokana na mazingira machafu.
Kamati ya bunge hilo kuhusu maji na mazingira ilipendekeza mpango wa kujengwa ukuta kwenye jaa la taka la Mwakirunge katika kaunti hiyo.
Akiongea bungeni humo siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kamati hiyo Bi Zainabu Mumba alisema kuwa pendekezo hilo ni kutokana na shinikizo kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo.
“Wakati tulipofanya ziara katika eneo hilo, wakaazi wa Mwakirunge walisema kuwa suluhu la kudumu ni kujenga ukuta katika jaa hilo. Hapo awali walikuwa wameleta pendekezo la kuwekwa mgao wa kifedha kushughulikia swala hilo,” alisema Bi Zainabu.
Mwenyekiti huyo aidha alisema kwamba wakaazi hao walipendekeza kuwa ujenzi huo utengewe mgao katika bajeti ya 2015 na 2016, lakini akasema kuwa jambo hilo halikufanyika.
Hata hivyo, Bi Zainabu aliwahakikishia kuwa katika bajeti ya 2016 na 2017 watazingatia zaidi mpango huo huku akiongeza kwamba kamati hiyo itafanya mjadala wazi na wakaazi kabla ya kuchukua hatua hiyo.
“Kabla kupitisha bajeti ya mwaka huu, lazima tutaenda kwa wananchi na mimi nawahimiza wakaazi wa Mwakirunge wasisitize kwamba mpango huo wa kujenga ukuta upewe kipau mbele,” alisema Bi Zainabu.
Bunge hilo lilisema kuwa ukuta huo utasaidia kuwakinga wakaazi wa eneo hilo dhidi ya kupata maradhi yanayotokana na athari za jaa hilo.
Wakati huo huo, bunge hilo lilipendekeza mpango wa kuweka tingatinga kadhaa za kuzoa taka katika eneo hilo ili kurahisisha shughuli hiyo.
Jaa la taka la Mwakirunge ni moja kati ya sehemu kubwa zaidi za kutupa taka mjini Mombasa, lakini kwa muda sasa wakaazi wa sehemu hiyo wamekuwa wakilalamikia harufu mbaya pamoja na wasiwasi wa kupata maradhi hatari.