Bunge la kaunti ya Nyamira limepitisha mswada wa kudhibiti muda wa kuhudumu kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya nyanjani almaarufu kwenye idara ya fedha katika serikali ya kaunti hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwasilisha hoja hiyo bungeni siku ya Jumatano, mwakilishi wadi ya Kiabonyoru James Sabwengi alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wanaosomea masomo hayo ya nyanjani kwenye idara hiyo wamekuwa wakihudumu kwa zaidi ya miezi inayotakikana, huku wakipewa marupurupu kila mwisho wa wiki hali inayoifanya serikali ya kaunti hii kupoteza pesa nyingi.

"Serikali ya kaunti hii imekuwa ikipoteza mamillioni ya pesa kwa kuwa pesa wanazopokezwa wanafunzi hao kila mwisho wa wiki ni pesa nyingi sana ambazo zinaweza tumika kufadhili miradi mbalimbali, na inawezekanaje kwamba kuna wanafunzi wanaohudumu kwenye idara hiyo kwenye masomo yao kwa zaidi ya miezi sita,"  aliuliza Sabwengi. 

Sabwengi aidha amesema kuwa sharti swala hilo lishughulikiwe kwa haraka kwa kuwa kuwepo kwa wanafunzi hao kwenye idara ya fedha kwa muda mrefu ni njia mojawapo ya kuwafanya kuwa wafanyikazi bila ya hata kuwepo na kandarasi.

"Sisi kama wawakilishi wadi sharti tulishughulikie swala hili kwa haraka kwa kuwa wanafunzi wanaohudumu kwenye idara hiyo wamefanywa kuwa wafanyikazi wanaolipwa hata bila ya kuwepo kandarasi," alisema Sabwengi. 

Akiunga mkono hoja hiyo, naibu kiongozi wa wachache kwenye bunge hilo Ken Atuti alisema kuwa kuwepo kwa muda mrefu kwa wanafunzi hao kwenye idara hiyo kunawazuia wanafunzi wengine kupata nafasi ya kuhudumu kwenye idara hiyo.

"Itawezekanaje kwamba wanafunzi wapewe nafasi ya kupata masomo ya nyanjani kwenye idara hiyo ya fedha kwa zaidi ya miezi sita huku wengine wanaotafuta nafasi za kupata mafunzo kwenye idara hiyo wakikosa nafasi," aliuliza Nyameino.