Bunge la kitaifa limeshinikizwa kulithamini swala zima la migogoro ya ardhi eneo la Pwani na kutafuta mbinu mbadala za kulisuluhisha swala hilo ili kuona kwamba mkaazi anafaidika.
Afisa wa kitengo cha dharura katika shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini la MUHURI Fahad Changi amesema kwamba ni lazima swala hilo la ardhi lishughulikiwe vyema mno ili kuepukana na mizozo.
Kulingana na Changi, eneo la Pwani limeathirika pakubwa na unyakuzi wa ardhi, huku serikali kuu ikikosa kutoa mwelekeo wowote licha ya wakazi kulishinikiza bunge kuingilia kati swala hilo na kuacha wakazi wakinyang’anywa ardhi zao kila uchao .
Aidha, mtetezi huyo wa haki za kibidamu nchini ameshinikiza kuvunjiliwa mbali kwa wizara ya ardhi nchini kwani haina umuhimu wowote katika kusawazisha migogoro ya ardhi katika taifa hili na hususan eneo zima la Pwani.
“Tumechoshwa na jinsi serikali na bunge la kitaifa linavyoshughulikia swala la mizozo ya ardhi hapa Pwani na kutuakikisha kama shirika la kutetea haki za kibinadamu tumeishinikiza vyema serikali na bunge kutatua mzozo huo ili mwananchi apate haki yake kikamilifu,” alisema Changi katika mkutano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi.
Kauli ya Changi inajiri baada ya wizara ya ardhi nchini kupata waziri mpya, Profesa Jacob Kaimenyi, aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta baada la rais kulifanyia baraza lake la mawaziri mabadiliko.