Zaidi ya walimu wastaafu 52,000 walio katika kundi la mwaka 1997, wamemtaka afisa mkuu katika tume ya kuwaajiri waalimu nchini TSC Nancy Macharia kusukumwa gerezani kwa wanadai ya kutotekeleza amri ya mahakama ya kuwalipa walimu hao pesa zao za pensheni.
Wakiongea mjini Nakuru Alhamisi, vinara wa walimu hao wastaafu wameelezea kugadhabishwa kwao na jinsi idara za serikali zinazofaa kutoa pesa hizo, zinavyojikokota katika kutekeleza amri ya mahakama.
Kulingana na mwenyekiti wao Charles Mwenje, zaidi ya walimu wastaafu 800 wameaga dunia wakingojea kupata haki zao hata baada ya kesi kufikishwa mahakamani, ambapo uamuzi uliotolewa 9/12/ 2015 uliwafaa walimu hao.
Ametaja hela zao kuingizwa kwa bajeti kwa miaka mitatu ya serikali sasa huku wakikosa ufahamu aliye na nia ya kuwakandamiza walimu hao kwa kuwanyima malipo yao.
“Sisi kama walalamishi na viongozi wa walimu wastaafu kundi la 1997, tunahisi kugadhabishwa na hulka ya idara za serikali ambazo zinafaa kutupa haki yetu kwa kutimiza amri ya mahakama,” alisema Mwenje.
Katibu wa muungano huo Gidraff Kimatta ambaye amesema kuwa hawatakubali viongozi wengine kuingilia kisiasa swala la wao kulipwa.
Walimu hao wanaidai serikali zaidi ya shilingi billion 42 sawia na riba zilizotokana na pesa hizo.