Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nyamira ameiomba serikali ya kitaifa kufanya uchunguzi upya kuhusiana na matumizi ya pesa za mayatima pamoja na wazee.

Share news tips with us here at Hivisasa

Alice Chae alidai kuwa pesa hizo zilizotengwa na serikali ya kitaifa ili kuwanufaisha mayatima na wazee wakongwe zinafujwa na watu wasio julikana.

Akihutubu kwenye makao ya mayatima kule Risa siku ya Alhamisi, Chae alisema kuwa idadi kubwa ya watoto mayatima na wakongwe haijanufaika kutokana na mpango huo, kwa madai kuwa pesa hizo zinawanufaisha baadhi ya watu wanaojifanya kuwa ndio wanao stahili kunufaika na mpango huo.

Aliipa serikali changamoto kufanya uchunguzi na kuwasilisha majina yawanaostahili kufadhiliwa.

"Pesa za wazee na mayatima hazitumiki kwa njia inayostahili na nataka serikali ifanye uchunguzi ili iweze kutengeza orodha ya watu wanaostahili kunufaika na pesa hizo. Kwa sasa kuna watu wanaovuja pesa hizo ilhali tunawafahamu vyema mayatima na wazee kwa kuwa hawa ni watu tunaoishi nao katika jamii,” alisema Chae.

Chae aidha alisema kuwa machifu na manaibu wao wanastahili kuchunguzwa kuhusiana na swala hilo na yeyote atakaye patikana kuwa na hatia afutwe kazi na kisha kuwasilishwa mahakamani.

"Tunakaribisha sana hatua ya serikali kuwafadhili mayatima na wazee katika jamii, ila ninashuku kuwa maafisa wa utawala hasa machifu na manaibu wao hawafanyi kazi yao inavyo stahili. Serikali inapaswa kuwachunguza na yeyote atakaye patikana na hatia, afutwe kazi na kushtakiwa mahakamani," aliongezea Chae.