Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha KANU katika eneo bunge la Malindi kupitia wanachama wake sasa wametangaza kujitoa kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi wa kiti cha ubunge wa Malindi.

Afisa wa chama cha KANU mjini Malindi Fuad Kombe ametangaza wazi kuwa chama hicho sasa hakitasimamisha mgombea yoyote kwenye kinyanganyiro hicho cha kiti cha ubunge.

Kombe amesema kuwa amri ya chama hicho kujitoa kwenye kinyanganyiro hicho imetoka kwenye afisi kuu za chama hicho jijini Nairobi, na kwamba wanajitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa 2017.

“Kama viongozi wa chama cha Kanu, tumeafikiana na viongozi wakuu wa chama chetu na kukubaliana kwa kauli moja kuwa hatutasimamisha mgombea yoyote bali tunapanga maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema Kombe wakati wa mahojiano na wanahabari siku ya Jumamosi katika ofisi cha chama hicho mjini Mombasa.

Uchaguzi huo mdogo wa Malindi umepangwa kufanyika tarehe 7 ya Machi kuwania kiti kilichoachwa wazi na Dan Kazungu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Madini nchini.