Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha maskauti katika Kaunti ya Kisii kitaanza kupita kwa mashule ya sekondari na vyuo kuwaelimisha vijana dhidi ya madhara ya mihadarati na pombe.

Hii ni baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya vijana ambao wamejihusisha na utumizi wa madawa za kulevya na pombe ni vijana wa shule.

Wanachama hao wa chama hicho cha maskauti walipokezwa mafunzo kupitia NACADA kuhusu ubaya wa utumizi wa pombe na madawa za kulevya, mafunzo ambayo watatumia kuwaelimisha vijana wengine katika mashule na vyuo.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Kisii, mwenyekiti wa chama cha maskauti hao Caleb Ondieki alisema kuanzia wiki ijayo Jumatatu wataanza kutembea kwa mashule ya sekondari na vyuo vyote katika Kaunti ya Kisii kuwaelimisha vijana dhidi ya madhara ya mihadarati na pombe ili kujitenga kutumia madawa hayo.

Ondieki alisema kuwa hii ni njia mojawapo ya mbinu za kuelimisha vijana kuhusu madhara ya madawa hayo katika jamii mbalimbali

“Mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kisii Richard Chebkawai ametupokeza barua ya kuturuhusu kupita kwa mashule kuwaelimisha wanafunzi ubaya na madhara ya kutumia dawa za kulevya na tutafanya hivyo kwanzia jumatatu wiki ijayo,” alisema Ondieki.

“Shirika la NACADA liliandaa mafuzo kwetu wanachama 60 dhidi ya utumizi wa madawa ya kulevya kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 16 mwezi wa kumi mwaka jana mafunzo ambayo sasa tutatumia kuwaelimisha vijana wengine katika mashule,” aliongezea Ondieki.

Aidha Ondieki aliwahimiza wakazi wengine wanaotumia mihadarati na pombe kuacha kwani zina madhara kwa miili zao.