Chama cha ODM huenda kikasambaratike zaidi katika eneo la Kisii kufuatia vurugu na udanganyifu unaoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, mwakilishi mteule katika kaunti ya Kisii Joyce Isaac alisema chama hicho kimekuwa 'ngome ya udanganyifu' wakati uchaguzi wa chama hicho unafanywa katika kaunti ya Kisii.
Kulingana naye, huenda chama hicho kipoteze uungwaji mkono katika eneo zima la Kisii ikiwa visa vya wizi haviadhibiwi mapema.
Mwakilishi huyo alisema kuna baadhi ya viongozi waliochaguliwa katika eneo bunge la Nyaribari Chache kuwa viongozi wa chama hicho na walikuwa wakifanya kampeini wakitumia gari za serikali huku wakiwaonga watu, jambo ambalo limewakera wengi na kusema ni wasaliti.
“Chama cha ODM kitasambaratika zaidi ikiwa visa vya aina hii ikiwemo udanganyifu vitaendelea kushuhudiwa hapa Kisii na kupoteza uungwaji mkono katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Isaac.
Waliokuwa wanawania nyadhifa za kuwa wenyekiti wa chama hicho katika eneo bunge la Nyaribari chache Bernard Ogari na Jackson Otegi walisema udanyifu ulishuhudiwa katika uchaguzi wa chama hicho, na kukikosoa chama cha ODM na kuitisha uchaguzi mwingine ili kuonyesha uwazi wa chama.