Chama cha TNA kimefungua afisi zake rasmi katika mtaa wa Kibera ulioko kaunti ya Nairobi huku kikijiandaa kujiimarisha kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa afisi hizo, katibu wa chama hicho katika eneo bunge la Kibera Awuor Obong'o amesema kuwa hatua ya kufungua afisi hiyo imeonyesha kukomaa kidemokrasia kwani kwa mda mrefu eneo la Kibra limekuwa likifahamika kama ngome kuu ya mrengo wa upinzani nchini Cord.
"Tukisheherekea kuzindua kwa ofisi hii mpya katika mtaa wa kibra, wacha iwe wazi kwa kila mmoja kuwa demokrasia imeimarika katika eneo hili la Kibra. Tuzingatie kwamba sisi wote tunasubiri kwa udi na uvumba kuzindua chama kikubwa cha vyama vinavyounga mkono mrengo wa Jubilee, chama ambacho kitatuelekeza kuzoa ushindi katika uchaguzi mkuu ujao," alisema Obong'o.
Tayari chama hicho kimewavutia wagombezi kadhaa wanaopania kuwania nyadhifa mbalimbali wakati wa uchaguzi huo mkuu akiwemo aliyekuwa diwani wa Sarang'ombe bwana Opete Opete ambaye amekigura chama cha ODM na kujiunga na TNA, chama tanzu chini ya chama kipya cha JAP.