Chama cha kutetea maslahi ya wafanyikazi wa mashamba makubwa makubwa nchini sasa kimejitokeza kusuta vikali ripoti zinazodai kwamba majadiliano ya pamoja ya mishahara ya wafanyikazi wa mashamba ya majani chai kati ya kampuni za chai na chama hicho sasa yatakuwa yakifanywa kila baada ya miaka minne na wala sio miwili.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira mapema Jumanne, katibu wa chama hicho tawi la Sotik Stephen Nyamweno alisema ripoti za aina hiyo ni mbinu ya watu fulani kuzua hofu miongoni mwa wafanyikazi, huku akisisitiza majadiliano ya wafanyikazi yatafanywa kama ilivyo kawaida.
"Ripoti ambazo zinaendelea kusambazwa miongoni mwa wafanyikazi kuwa majadiliano ya mishahara ya wafanyikazi yatakuwa yakifanywa kila baada ya miaka minne ni ya uongo kwa maana tutakuwa tukifanya majadiliano hayo kila baada ya miaka miwili ilivyokuwa hapo awali," alisema Nyameino.
Nyamweno aidha aliziomba serikali za Kaunti ya Nyamira, Kericho na Bomet kutafuta namna ya kuzisurutisha kampuni za chai kuacha kutumia mashine za kuchuna chai maana mashine hizo zimelazimu kampuni nyingi za chai kuwaachisha kazi wafanyikazi wake.
"Ni ombi langu kwa serikali za kaunti kuhakikisha kuwa wanazishurutisha kampuni za chai kuasi matumizi ya mashine za kuchuna chai kwa kuwa utumizi wa mashine hizo umewafanya waajiri wengi kuwafuta kazi wafanyikazi wengi," aliongezea Nyameino.