Baada ya tetesi kali kuibuliwa dhidi ya shule mbalimbali za umma kuongeza karo za shule bila kuwashauri washikadau, chama cha wazazi nchini tawi la Nyamira kimejitokeza kushtumu vikali hatua hiyo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira, Mwenyekiti wa chama hicho tawi la Nyamira Vincent Mbura alisema shule mbalimbali zimekiuka kiwango cha karo kilichotolewa na serikali na kupandisha karo bila ya kuwashauri washikadau husika. 

"Ni jambo lakushangaza kuwa baadhi ya walimu wakuu wa shule wamekiuka agizo la serikali la kutoongeza karo kiholela, na hii ni mbinu mojawapo ya kuwanyanyasa wazazi wa taifa hili," alisema Mbura. 

Mbura aidha amewahimiza wazazi kutolipa viwango hivyo vya karo huku akisema kuwa iwapo bodi za shule hazitoketi na washikadau na kurekebisha viwango vipya vya karo, chama cha kitaifa cha wazazi kitawasilisha kesi mahakamani mapema Januari kupinga hatua hiyo anayosema imekuwa mzigo mkubwa kwa wazazi. 

"Ningependa kuwahimiza wazazi wenzangu kutokubali kulipa viwango hivyo vipya vya karo kwa kuwa hiyo ni kinyume na sheria, na iwapo usimamizi wa shule mbalimbali hautoketi na washikadau na kurekebisha viwango hivyo, basi na wajue kuwa chama cha wazazi kitawasilisha kesi mahakamani kupinga hatua hiyo," alionya Mbura.