Share news tips with us here at Hivisasa

Huku baadhi ya wakazi wa eneo la Likoni wakipokezwa hatimiliki za ardhi katika eneo la Waitiki siku ya Jumamosi, mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kwale amemtaka Rais Uhuru kutafuta njia mwafaka ya kutafuta suluu la kuwapa fidia wenye ardhi katika eneo la Dongo Kundu.

Akiongea katika eneo la Shika Adabu siku ya Jumamosi katika wilaya ya Likoni, Kaunti ya Mombasa, Mwakilishi huyo Zainabu Chidzuga, amesema kuwa kuna baadhi ya watu ambao anadai wana hatimiliki lakini maeneo ya ardhi na mashamba si yao.

Mwakilishi huyo alimtaka rais Uhuru kuunda jopo ili kuanza kuwachunguza matapeli ambao anasema wameanza kuongezeka katika eneo hilo la Dongo Kundu ili kufahamika wamiliki halisi wa ardhi katika eneo hilo.

“Kuna watu ambao wanaendelea na ulaghai wa maeneo ya ardhi katika eneo la Dongo Kundu na sharti wafanyiwe uchunguzi Bwana rais, kuna watu wana hatimiliki lakini si wamiliki halisi wa ardhi,” alisema mwakilishi huyo.

Maeneo mengi ya Pwani yamekuwa na mizozo ya mara kwa mara ambayo inahusisha mabwanyenye kunyakua mashamba ya wakazi na wenyeji wa maeneo hayo ambako wengi wamebaki kuwa masikwota katika ardhi yao.