Baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa Cord, katika eneo la Pwani wamewasihi wakaazi wa Malindi kutokubali kuhongwa kwenye uchaguzi mdogo wa Malindi utakao kuwa Machi mwaka huu.
Wakiongozwa na mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga, viongozi hao waliwaonya wakaazi dhidi ya kupokea hongo kwa kudai kuwa kuna njama ya kuhonga wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa Malindi.
Akizungumza siku ya Jumamosi, wakati wa hafla ya mchango wa wanafunzi huko Kijiwetanga kaunti ndogo ya Malindi, Chidzuga alidai kuwa kuna watu wanaopanga kutoa pesa kwa wananchi kwa malengo ya kuvichukua vitambulisho vyao vya kitaifa ili wasishiriki kura hizo.
Chidzuga aliwataka wanawake kutoshawishiwa kwa pesa ili kumchagua kiongozi bali kuwa mstari wa mbele katika kumchagua kiongozi anayefaa.
Mbunge wa Lamu Magharibi Ali Athman alikosoa serikali zilizotangulia akisema hazikuwatambua Wapwani kimaendeleo kama inavyofanya serikali ya Jubilee.
Kauli hii inajiri baada ya joto la siasa kuchacha katika eneo la Malindi, huku uchaguzi mdogo ukiwadia.