Chifu wa lokesheni ya Bisiongororo Kaunti ya Kisii Robert Isoe amewashauri wazazi wote wa kaunti hiyo ambao wanao walipata alama ya zaidi ya 350 katika mtihani wa darasa la nane mwaka jana kujaza fomu ya benki ya Equity na ile ya Family ili kufadhili watoto hao kimasomo.
Hii ni baada ya benki hizo mbili kujitolea kufadhili watoto waliopata alama ya zaidi ya 350 ili kuwafadhili watoto haswa wasiojiweza.
Kulingana na chifu huyo, hakuna haja ya wazazi kukawia kujaza fomu hizo kwani ufadhili wa masomo uko ili kusaidia watoto kujiendeleza kielimu.
Akizungumza na mwandishi huyu wa habari siku ya Alhamisi mjini Kisii, chifu Isoe aliomba wazazi kuwajibika haraka ili kuwasaidia wanao.
“Benki zimejitolea kusaidia watoto kuendeleza masomo, hakuna haja ya mzazi kutofikia kwa benki hizo ili kutafuta msaada huo, naomba wote wafanye hivyo ili tupunguze umaskini katika jamii yetu ya Kisii,” alisema Isoe.
Wakati huo huo, chifu huyo aliomba wazazi kuwasomesha wanao na kutouza mashamba yao na kununulia wanao pikipiki ili kuendesha kabla ya kumaliza masomo.
Isoe alisema kuwa imeripotiwa kuwa kuna wazazi huuza mashamba yao na kununulia watoto wao pikipiki baada ya kumaliza darasa la nane, na kusema hiyo ni njia moja ya kuwanyima watoto haki ya masomo na kuongeza umaskini.