Chifu wa kata ya Keera, katika kaunti ya Nyamira John Oire amejitokeza kuwaonya vikali wagemaji na wabugiaji pombe haramu katika eneo lake. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubia wanahabari katika hafla ya kuwazawadi wanafunzi waliofanya vyema kwenye mtihani wa darasa la nane kule Nyaisa siku ya Ijumaa, Oire alisema kuwa ameweka mikakati ya kuwapeleka mahakamani watakaopatikana kuhusika pakubwa.

"Nimeweka mikakati kuhakikisha kwamba watu watakaopatikana wakigema na hata kunywa pombe haramu wanafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka kwa maana hali hii inaathiri pakubwa ukuaji wa eneo hili kiuchumi," alisema Oire. 

Oire aidha aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kuwekeza pakubwa kwenye elimu ili kusaidia eneo hilo kuimarika pakubwa kiuchumi, hali aliyosema itasaidia kupunguza visa vya uhalifu katika eneo hilo.

"Ni himizo langu kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba wanawaelimisha wanao ili kustawisha eneo hili kimaendeleo kwa maana nina hakika kuwa hali hii itasaidia kupunguza visa vya uhalifu," aliongezea Oire.