Chifu wa Bokeng’oina, kaunti ya Kisii amewataka wazazi kuhakikisha wanao ambao ni wanafunzi wamekuwa waadilifu kwenye likizo ya Disemba ili kuepuka anasa na maovu katika jamii shule zinapoendelea kusalia kufungwa.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Kisii chifu Shadrack Chogoro amewataka wazazi kutoa ulinzi na kuwajibika kwa wanao ili kuwaepusha na matembezi ya kiholela na badala yake kurejelea masomo wakati huu wa likizo.
"Naomba wazazi wote hapa Kisii kuwashauri wanao ambao ni wanafunzi kusalia manyumbani mwao wakati huu wa likizo ya Disemba ili wasije wakapata madhara wanapofanya matembezi kiholela ,” alisema Chogoro chifu wa lokesheni ya Bokeng’oina .
"Sharti wazazi wahakikishe wanao wanasoma likizo inapoendelea ili wasije wakasahau kwa haraka silabasi kwani likizo hii ni refu,” aliongeza chifu.
Hata hivyo, chifu huyo aliwatahadharisha wazazi dhidi ya kuwahusisha wanao kwa kazi zinazoweza kuwaathiri kiakili kwani Januari mwaka ujao watarudi shuleni.
Kulingana na chifu huyo, kwa mara nyingi shule zinapofungwa idadi kubwa ya wanafunzi katika maeneo mengi hupatikana wakirandaranda sokoni na katika barabara wakiwa wametumwa na wazazi kununua na kuuza bidhaa mbalimbali jambo ambalo chifu huyo amelikashifu na kuwaonya wazazi dhidi ya jambo hilo.
“Kila mzazi anastahili kufuatilia hatua ya mtoto wake, na matembezi ya watoto kwenye soko bila sababu muhimu huchangia sana utovu wa nidhamu miongoni mwao, na naomba hilo likomeshwe,” alionya chifu Chogoro.