Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wito umetolewa kwa wanachama wa kundi la MRC eneo la Pwani kujitokeza na kujisajili kama wapiga kura, ili kuwa ange kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kundi hilo limetakiwa kuchangamkia shughuli hiyo inayoendelea kote nchini ili kuhakikisha kuwa wanaungana na wapwani wengine kuleta mageuzi katika taifa hili.

Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa chama cha Wiper aliye pia mmoja wa vigogo katika muungano wa Cord, Kalonzo Musyoka akiwa katika ziara ya siku mbili eneo hilo.

Akiongea katika uwanja wa Caltex, wilayani Likoni siku ya Jumapili, Kalonzo amelitaka kundi hilo kutumia fursa hiyo kusafisha jina lao ambalo limekuwa likihusishwa na visa vya fujo na ukatili.

"Ningependa kuwaambia hawa vijana wa MRC, huu ni wakati wenu sasa mchukue kadi za kupiga kura ili mbadilishe eneo letu kimaendeleo," alisema Kalonzo.

Kauli ya kiongozi huyo inakuja siku kadhaa baada ya tetesi kuibuka  kwamba kundi hilo lilikuwa likipanga kuvuruga zoezi hilo la kusajili wapiga kura.

Wakati huo huo pia, Kalonzo alichukua nafasi hiyo kuwahimiza wakaazi wa Pwani kuhusu umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura akisema hiyo ndio njia pekee ya kujinasua kutoka katika uongozi mbaya unaoendesha na wanasiasa fisadi.