Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amewahimiza wakazi wa enei ka Pwani kujisajili kwa wingi kama wapiga kura, akihoji kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee itakayouwezesha muungano wa Cord kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano jioni, Joho aliutaja ushindi wa chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi kama ishara tosha kuwa Cord ingala na umaarufu Mkoani humo, na kuwa itazoa kura zote katika uchaguziwa 2017.
‘’Tuliwabwaga Malindi, kila mtu ameona. Bado 2017 sasa tuingie Ikulu. Nawasihi mchukue kura kwa wingi ili tuweze kuleta mabadiliko ya uongozi nchini,’’ alisema Joho.
Aidha, Joho alisema kuwa wabunge waasi wa muungano wa Cord kutoka ukanda wa Pwani waliohamia Jubilee hawawezi kuyumbisha uthabiti wa muungano huo Mkoani humo kwani nia yao ni kujinufaisha badala ya kutetea haki za wakazi.
‘’Walivuka ule upande mwingine wakidhani watatuangusha, sasa wamekosa la kusema baada ya kuonyeshwa kivumbi,’’ aliongeza Joho.
Picha: Gavana wa Mombasa Ali Joho akisherekea ushindi wa chama cha Cord katika kiti cha Malindi. Joho anawataka wakazi kujiandikisha kwa wingi kuwa wapiga kura. Thestar.co.ke