Kufuatia ripoti zilizochapishwa kwenye magazeti ya humu nchini kuwa tume ya elimu ya vyuo vikuu CUE  yataka kufunga baadhi ya matawi ya chuo kikuu cha Kisii kutokana na kutoafikia matakwa fulani, sasa chuo hicho kimejitokeza kusuta vikali ripoti hizo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumatano, afisa mshirikishi wa chuo hicho tawi la Nyamira Eliud Nyakundi alisema chuo hicho hakijapokea ripoti zozote kutoka kwa tume hiyo kuhusiana na madai ya chuo hicho kuhitajika kufunga baadhi ya matawi yake. 

"Kumekuwa na ripoti zilizochapishwa kwenye magazeti ya humu nchini na hata kwa vyombo vya mawasiliano ya kijamii kuwa chuo chetu kinahitajika kufunga matawi kumi kati ya kumi na tatu kwa kutoafikia vigezo fulani ila sisi hatujapokea ripoti zozote za tume hiyo kututaka kufanya hivyo," alisema Nyakundi. 

Nyakundi aidha amewahimiza wanafunzi wa chuo hicho kutokuwa na hofu huku akiwasihi kuendelea na shughuli zao za kawaida usimamizi wa chuo hicho unapotafuta suluhu la suala hilo. 

"Ningependa kuwahimiza wanafunzi wetu kokote walipo kutokuwa na hofu ya kuathirika kivyovyote na ripoti hizi kwa kuwa usimamizi wa chuo utafuatilia suala hili kukuhakikisha kuwa limesuluhishwa," aliongezea Nyakundi.