Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK limepongeza hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuutatua mzozo wa ardhi katika Shamba la Waitiki la hekari 930 kwa kutoa hati miliki kwa wakazi hao eneo la Likoni.
Katibu Mtendaji katika baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa amesema kuwa hatua hiyo imeonyesha wazi kuwa serikali inajali maslahi ya wakenya wa mashinani na imejitolea kutatua mzozo wa ardhi katika eneo zima la Pwani.
Kwenye kikao na wanahabari katika afisi za baraza hilo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Sheikh Khalifa amewataka wakazi wa Shamba la Waitiki kujiepusha na baadhi ya viongozi wa kisiasa wanatumia fursa hiyo kisiasa ili kupotosha wakazi na kuvuga amani katika eneo hilo.
"Tunawaomba viongozi wa kisiasa kutolichukulia swala la Waitiki kisiasa na kuanza kuwagonganisha wakenya kwa sababu hatua hiyo huenda ikasambaratisha shughuli za kiusalama, na nawasihi vijana kujiepusha na watu kama hao na kutumia fursa hiyo kuweka amani," alieleza Sheikh Khalifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo Abdallah Ateka ameunga mkono kauli ya Sheikh Khalifa na akawataka wakazi wa eneo hilo kuzitumia vyema hati miliki hizo katika kujiendleza kimaendeleo.
"Tunatoa wito kwa wakazi wa Shamba la Waitiki, Rais alifanya jambo jema na sisi tunawahimiza wakazi kuhakikisha kuwa watumia fursa ya hati miliki hizo walizopewa kufanya miradi ya kimaendeleo kwa kutafuta," alisema Sheikh Ateka.
Kuali ya viongozi hao wa kidini imejiri siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa hati miliki 5,700 kwa wakazi wa shamba la Waitiki eneo la Likoni lililokuwa na mzozo wa miaka mingi.